WAKURUGENZI WAPEWA MWEZI MMOJA KUKAMILISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA SHULE ZA WASICHANA

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa mwezi mmoja kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule mpya za sekondari za bweni za wasichana za mikoa ambazo zimejengwa katika halmashauri zao ili wanafunzi walioripoti katika shule hizo wapate mazingira bora na rafiki ya kupata elimu.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akipokea taarifa za ujenzi wa shule hizo 26 za sekondari za wasichana za mikoa wakati wa kikao cha tathmini ya ujenzi wa shule hizo kilichofanyika katika Ukumbi wa Arnautoglo wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mchengerwa amesema, alitegemea wakurugenzi watoe taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa shule hizo kwa asilimia 100 jambo ambalo halijatekelezeka, wakati yeye akiwa kwenye ziara ya Mhe. Rais Mkoani Rukwa alimuahidi Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ndani ya mwezi mmoja miundombinu ya shule zote 26 itakuwa imekamilika.

Waziri Mchengerwa ameanisha kuwa, wapo wakurugenzi amewapatia wiki mbili, wiki tatu na wengine mwezi mmoja wa kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miundombinu iliyosalia katika shule hizo za wasichana za mikoa, isipokuwa mkurugenzi anayesimamia ujenzi wa shule ya mkoa wa Rukwa ambaye amempatia miezi 2.

“Hakutakuwa na nyongeza ya muda katika kipindi ambacho tumekubaliana mkamilishe ujenzi wa miundombinu ya shule hizo, na sitosita kumchukulia hatua mkurugenzi yeyote atakayeshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule kwa mujibu wa makubaliano yetu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, yeye binafsi pamoja na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wanawategemea wakurugenzi hao katika usimamizi wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Bw. Kagurumjuli Titus amesema kwamba wamepokea maelekezo ya Waziri Mchengerwa na kuhaidi kuwa, manispaa yake itakamilisha ndani ya siku 15 hadi 21 ujenzi wa miundombinu ya shule ya mkoa ya Dar es Salaam ambayo ilikuwa haijakamilika kwani Mhe. Rais ameshawapatia fedha.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma Bi. Mariam Chaurembo amesema kuwa, Halmashauri yake kwa niaba ya mkoa wa Songwe imejipanga kutekeleza maelekezo na Waziri Mchengerwa ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Songe ndani ya mwezi mmoja kama alivyoelekeza.

Kikao hicho cha tathmini ya ujenzi wa shule 26 za sekondari za wasichana za mikoa, kimeudhuriwa na Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Elimu wa Sekondari, Wahandisi wa Halmashauri na Maafisa manunuzi wa Halmashauri.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم

TUTUMIE UJUMBE HAPA