YESU ALIKAMATWA NA KUTESWA KINYUME CHA SHERIA KABLA YA KUFIKISHWA MBELE YA PILATO


 

Je, ni watu gani waliomkamata Yesu usiku ule wa Alhamisi Kuu? Je, watu gani waliohusika na mateso yake? Je, watu gani waliomsulubisha? Haya ni baadhi ya mambo yanayowachanganya watu wengi wakiwemo hata baadhi ya wahubiri ambao ubobezi wao katika Biblia ni mdogo.

Mathayo anashuhudia kuwa umati wa watu walioshika panga na rungu walifika kumkamata Yesu na kuwa walitumwa na makuhani wakuu pamoja na wazee wa watu  (Mathayo 26:47).

Ushahidi wa Marko unasema kuwa umati wa watu wakiwa na panga na rungu walimkamata Yesu na kuwa walitumwa na makuhani wakuu, walimu wa sheria na wazee (Marko 14:43).

Luka anataja umati mkubwa bila kueleza silaha walizoshika. Lakini ushahidi wake unaonyesha walikuwa ni askari waliokuwa wakilinda hekalu na baadhi walikuwa ni watumishi wa makuhani (Luka 22:47;50). Lakini Luka anatuongeza kitu cha ziada katika ushahidi wake kuwa miongoni mwa umati ule walikuwemo makuhani wakuu na wazee (Luka 22: 50).

Yohana anashuhudia kuwa kikosi cha Askari na maafisa kutoka kwa makuhani wakuu na mafarisayo walifika kumkamata Yesu wakiwa na mienge, vibatari na silaha (Yohana 18:2-3).

Ushahidi wa waandishi wote wa sinoptikia (the synoptic gospels writers - Mathew, Mark and Luke) na ushahidi wa Yohana unaoana kuwa Yesu alikamatwa na Mamlaka ya Kiyahudi kwa maamuzi halali ya Baraza Kuu la Utawala wa Kiyahudi (Sanhedrin).

Hivyo, mateso, matusi, manyanyaso ambayo Yesu aliyapata kabla hajapelekwa kwa Pilato yaliamriwa, yalifanywa na hata kusimamiwa na Mamlaka ya Kiyahudi. Ni kama vile mtuhumiwa anavyoteswa anapokamatwa na Jeshi la Polisi na pia anapokuwa katika mahabusu ya Polisi kabla hajapelekwa mahakamani. Kama ilivyo ni haramu kwa sasa Polisi kumtesa mtuhumiwa, ilikuwa ni haramu kwa Mamlaka ya Kiyahudi kumtesa mtuhumiwa bila ya kumpeleka kwa Pilato ili kupata kibari.

Kwa sababu hiyo, mateso yote aliyopata Yesu alipokuwa mikononi mea mamlaka ya Kiyahudi yalikuwa ni haramu. Ushahidi wa kuwa Yesu aliteswa akiwa mikononi mwa mamlaka hiyo uko wazi. Mathayo anatoa ushuhudia kuwa Yesu alipokuwa mbele ya Baraza la Sanhedrin alitemewa mate, alipigwa ngumi na kupigwa makofi (Mathayo 26:67). Mathayo anashuhudia zaidi kuwa Yesu alifungwa pingu na kuburuzwa hadi kwa Pilato (Mathayo 27:2).

Marko anashuhudia kuwa alipokuwa mbele ya Sanhedrin, Yesu alitemewa mate, alifungwa kitambaa usoni, alipigwa ngumi na baadaye pia walinzi waliendelea kumpiga (Marko 14:65). Na hata Marko anashuhudia kuwa Yesu alifungwa pingu mikononi na kupelekwa mbele ya Pilato (Marko 15:1). Ikumbukwe kuwa hata kumfunga mtuhumiwa kitambaa usoni na hata kumfunga pingu, hiyo ni sehemu ya mateso.

Luka anashuhudia kuwa walinzi walianza kwa kumdhihaki na kumpiga, walimfunga kitambaa usoni na walimtukana matusi mazito (Luka 22:63-65). Luka anaongeza ushahidi wa ziada kuwa hata alipopelekwwa mbele ya Herode, na kule pia alitukanwa na kudhalilishwa na Herode pamoja na askari wake (Luka 23:11).

Yohana anashuhudia kuwa Yesu alipopelekwa mbele ya Anasi aliyekuwa ndiye Kuhani Mkuu mstaafu, alipigwa na Afisa mmoja na kisha akapelekwa mbele ya Kayafa ambaye alikuwa ndiye Kuhani Mkuu. Muda wote akiwa mbele ya Anasi alikuwa amefungwa (Yohana 18:22).

Ikumbukwe kuwa, muda wote huo na mateso yote hayo aliyopata alipokuwa mikononi mwa Baraza la Kiyahudi, hiyo haikuhesabiwa kama sehemu ya kusulibishwa kwa sababu alikuwa bado hajafika mbele ya Pilato na hivyo alikuwa bado hajahukumiwa. Kusulubishwa ilikuwa ni hukumu halali iliyotolewa na mahakama chini Pilato ambaye aliyekuwa jaji mwenye mamlaka ya kutoa na kupitisha hukumu ya kifo.

Kwa hiyo, Yesu aliteswa sana kinyume cha sheria kabla hata hajafikishwa mahakamani. Ni sawaswa na watuhumiwa wengi sasa ambao pia huteswa na hata kufia mikononi wa Polisi kinyume cha sheria kabla hata hawajafikishwa mahakamani.  

Bwana Yesu alikamatwa kinyume cha sheria kwani sheria ya Kirumi ilikataza kumkamata mtuhumiwa asiye mharifu wa ujambazi usiku. Unaweza kuona jinsi Yesu aliwashangaa ni kwa nini walimjia usiku wakati yeye hakuwa ni jambazi. Pia, Yesu aliteswa kinyume cha sheria akiwa mikononi wa Mamlaka ya Kiyahudi kwani sheria za Kirumi hazikuruhusu utesaji ule.

Baada ya kueleza hatua hii ya ukamataji wa kinyume cha sheria na utesaji ulio kinyume cha sheria, sasa tutaendelea kueleza hasa kuhusu mateso ya Yesu baada ya kuhukumiwa na mahakama halali ya Pilato. Mchakato huo ndio unaoitwa kulubisha. Je, ulikuwa unajua haya? Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki
Dar es Salaam

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA