HII HAPA RATIBA YA ZIARA YA WAZIRI MKUU MHE. MAJALIWA MKOANI MARA

Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa

 MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda ametoa taarifa ya ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majali Mkoani humo kuanzia leo Februari 25 hadi 29, 2024.


Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake mjini Musoma jana, Mtanda alisema katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa anatarajiwa kuzungumza na watumishi na viongozi, kufanya mikutano ya hadhara, kutembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za utawala, elimu, afya na miundombinu.

“Maandalizi ya ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Mkoa wa Mara yamekamilika. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi, watumishi na viongozi wa ngazi mbalimbali walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha maandalizi ya ziara hii,” Amesema RC Mtanda

RC Mtanda alisema mapokezi ya Waziri Mkuu kimkoa yataanzia Ndabaka Wilayani Bunda leo mchana, kisha ataelekea Ukumbi wa Uwekezaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Musoma kwa ajili ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Mkoa, kesho Februari 26, Waziri Mkuu Majaliwa atasalimia wananchi wa Mariwanda kabla ya kutembelea na kukagua Shule ya Msingi Sabasita katika eneo hilo, kisha atakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Baadaye Waziri Mkuu atakagua na kuzindua mradi wa maji wa Sazira na kufanya kikao na watumishi na viongozi kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Miembeni, Bunda Mjini.

Mtanda amesema Februari 27, kiongozi huyo wa kitaifa atakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, kufanya kikao na watumishi na viongozi, kuwasalimia wananchi na kuzuru nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo, Butiama.

“Aidha, Waziri Mkuu atafanya kikao na watumishi na viongozi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sokoine, Mugumu na baadaye kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Getarungu.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu ataelekea Nyamwaga ambapo ataweka jiwe la msingi katika jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kusalimiana na wananchi,” alisema Mtanda.

Mkuu huyo wa mkoa alisema Februari 28, Waziri Mkuu Majaliwa atatembelea na kukagua mradi wa maji Komuge na baadaye kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Utegi.

Baadaye Majaliwa atahutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Sirari na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa soko la kimkakati la Mji wa Tarime kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Serengeti katika Mji wa Tarime.

Februari 29, Waziri Mkuu atakagua ujenzi wa Uwanja wa Ndege Musoma, kisha kuelekea kijiji cha Suguti kuweka jiwe la msingi katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kabla ya kuzungumza na viongozi na watumishi.

Kulingana na ratiba hiyo, Waziri Mkuu atakwenda kijiji cha Bwai (Bwai Kumsoma) kwa ajili ya kuzungumza na wananchi katika uwanja kijijini hapo na kuhitimisha ziara yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, ambapo atafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Sekondari Mara.

Hivyo RC Mtanda amewaomba wananchi husika kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi na mikutano ya hadhara iliyopangwa karibu na maeneo yao.
Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA