UCHUMI SHINDANI WA VIWANDA CHACHU YA TANZANIA KUWA NCHI YA KIPATO CHA KATI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 28 Oktoba, 2023 amehitimisha rasmi Maonesho ya Shirika la Viwanda vidogo vidogo (SIDO) yaliyofanyika katika Viwanja vya Sabasaba  katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Mkoani Njombe.


Dkt. Philip Mpango aliwasili viwanjani hapo na kuanza kutembelea  mabanda mbali mbali ya maonesho ya bidhaa za Wajasiliamali hao na kujionea ubunifu tofauti katika Sekta ya Viwanda hapa nchini.

" Mpango wa Taifa wa  Maendeleo wa miaka mitano tunaoutekeleza hivi sasa  unatutaka tukuze  mchango wa Uchumi  pamoja na Ajira zinazotokana na Viwanda katika pato la Taifa. Hivi sasa mchango wa Sekta ya Viwanda ni asilimia 7.1 tunatamani tufikie asilimia 9 ifikapo mwaka 2025 hadi 2026". Amesema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango amesisitiza kuwa, tafiti zina umuhimu mkubwa sana katika kukuza matumizi ya teknolojia mbali mbali kwenye Uzalishaji na uongezaji thamani wa  bidhaa na mazao.


Katika Maonesho hayo ambayo Tume ya Madini ilishiriki, akizungumza mara baada ya kutembelea banda la Tume ya Madini. Dkt. Mpango amewataka Watendaji wa Tume ya madini kufanya utafiti ili kujua madini yapi yanapatikana eneo gani? na kuhakikisha takwimu mbali mbali zinapatikana hapa nchini ili kuongeza Pato la Taifa.


Dkt. Mpango amesema kuwa, maonesho ya SIDO yameshirikisha Wajasiliamali 628 na teknolojia 95 ambazo zinatumika kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao mbali mbali ikiwemo Parachichi  linalozalishwa kwa wingi Mkoani Njombe.


Aidha, Dkt Mpango ameelezea kufurahishwa kwake na kauli mbiu ya Maonesho hayo ambayo inasema "kwa Pamoja tujenge Viwanda kwa Uchumi na Ajira  endelevu" na kusema, Kauli hii iwahamasishe watu wote hasa vijana kuingia kwenye Sekta ya Kilimo, Viwanda na Biashara.


Akizungumza katika Maonesho hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema, Maonesho ya nne ya Wajasiliamali yamekuwa na ongezeko  kubwa la washiriki ambapo mwaka 2018 walihudhuria Wajasiliamali 582 yalipofanyika  kwa mara ya kwanza Mkoani Simiyu na mwaka 2023 idadi ya  washiriki imeongezeka kufikia Washiriki 628.


Hafla ya kilele cha Maonesho hayo ambayo yamefikia tamati tarehe 28 Oktoba, 2023, yamehudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Sekta Binafsi, Viongozi wa dini, Wajasiliamali pamoja na Wananchi.

Je?, UNA HABARI,PICHA, TANGAZO AU TAARIFA AMBAYO UNGEPENDA TUICHAPISHE KATIKA MTANDAO HUU? WASILIANA NASI, Email : fichuziblog@gmail.com , Simu +255 752 925 603

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post

TUTUMIE UJUMBE HAPA